===================THIS IS MY STORY=============
JUMAPILI 06 April, 2014...... (Ufufuo na Uzima - Morogoro)
USHUHUDA WA LEO: THIS IS MY STORY, BY CESILIA (Part One)
Utangulizi: Cesilia Alilkuwa ameolewa Tanga na mwanaume ambaye alikuwa
mganga wa kienyeji, ila hakuwahi kumweleza ukweli kuwa ni mganga.
Alipata ujauzito uliodumu kwa miezi 12 na kisha akaamua kwenda kwa
mganga wa kienyeji kuaguliwa. Mganga akamwambia anatakiwa apatiwe dawa
ya kuishusha nyota yake. Alimletea dawa ambayo ni mavi ya tembo, ambayo
alitakiwa akoroge hiyo dawa nyakati za saa nane usiku ainywe. Alitakiwa
atumie sumaku kuishusha hiyo dawa kuanzia kifuani hadi tumboni ili hapo
kesho yake aweze kujifungua. Hata hivyo ilipofika kesho yake
hakujifungua.
Wengine walimwambia aende kwa bibi yake
kijijini. Bibi huyo alimpeleka kwa mkunga. Mkunga alimwambia inaelekea
hiyo mimba ni kubwa sana, ila anachotakiwa ni kuwa akipata tu uchungu
aende hospitali. Cesilia aligoma kwenda hospitali akisema “kama ni kufa
na nife tu”, haya aliyasema akiwa nyumbani kwake.
Siku ya siku
ililazimu kwenda hospitalini, ambapo walimwambia inaelekea ana mimba ya
Watoto wanne. Hata hivyo hospitalini pale manesi walikuwa
wananong’onezana wao kwa wao kwamba huyu mgonjwa ni wa kufa, na hakuna
uwezekano wa kupona. Pale hospitalini madktari waliitana na kumwambia
asaini hati ya kufanyiwa operesheni. Wakati wa kufanyiwa ile operesheni,
ghafla alikosa fahamu, kisha akajikuta yupo mahali ambapo wamejaa
Waarabu, na walikuwa wanachezea midoli. Waarabu hawa Walikuwa
wakimlazimisha apokee hiyo midoli, lakini akakataa. Baada ya kuzinduka
usingizini, alimkuta mdogo wake pembeni mwa kitanda. Alimuuliza dada
yake kipi kinaendelea akaambiwa, tayari ameshafanyiwa operesheni na
mtoto wako yupo kwa manesi. Aliomba kupatiwa mtoto amuone, lakini
alipoletewa kumuona, alishangaa kumuona mtoto wake kuwa na kichwa
kikubwa sana. Mtoto huyu alikuwa mlemavu kiasi kwamba hawezi kugeuza
kichwa chake.
Ndani ya Mwezi mmoja wa kuishi kwa yule mtoto
tayari alikuwa na uwezo wa kuongea maneno kama ‘mama hamna, baba,
babu’….. Huyu mtoto nyakati nyingine alikuwa na vituko kiasi kwamba
majirani wa kiislamu walikuwa wanamtia moyo mama huyu, eti katika dini
yao Watoto kama hao wapo, na ni maalumu kwa kutoa shuhuda. Pamoja na
kwamba mtoto huyu alikuwa hawezi kujiegeuza, lakini nyakati za usiku
mama yake alikuwa akiamka anamkuta huyu mtoto akiwa kwenye titi
ananyonya, na akawa anajiuliza ni nani anayemsaidia kumweka mtoto
kwenye titi bila kupata majibu.......!!!!
Siku moja alitokewa na
majini matano. Hawa walikuwa wamevaa baibui, wakamtishia wakisema, “wewe
ni wifi yetu, uliolewa na kaka yetu, na sasa hutaki kumleaa huyu
mtoto. Kuna siku tutakuja kumchukua huyu mtoto, tutakupa pesa, na
ukifanya mchezo tutaondoka na wewe pia ili ukamlee huyu mtoto”. Walimpa
Tarehe na muda wa kuja kumchukua huyu mtoto. Siku tatu kabla ya Tarehe
majini waliyosema ni ya kumchukua mtoto huyu, alipata wazo la
kuchangisha michango akitumia picha ya yule mtoto ili mtoto akapatiwe
matibabu ya kichwa chake. Waliomshauri walimwambia apite kwenye maduka
ya WAARABU na WAHINDI kwani ni wazuri sana kwenye kuchangia mambo kama
haya, naye akafanya hivyo.
Mama alivyorudi aliambiwa mwanao
amekunywa maziwa kikombe lakini papo hapo akatapika puani mitihili ya
maji maji. Mama alimuitaa mwanae kwa jina lake la Robert, naye
akamuitikia mama yake, huku akimpangusa machozi mama yake. Hata hivyo
alikufa baadae kidogo na kupelekwa kijijini kwa mazishi, wakitumia pesa
ile ya michango ya jana yake, sawasawa na lile neno aliloambiwa na yale
majini kuwa watampatia pesa. Walifanya mazishi ya haraka haraka nyakati
za usiku kwani waliokuja pale walishauri maiti asikae muda mrefu kwani
alikuwa anaumuka na kuongezeka umbile lake. Bwana wake alikasirika sana
mwanae huyu kuzikwa mahali nje ya Njombe kwani alikuwa ni mzaliwa wake
wa kwanza.
Bwana wake alianza kujidhihirisha kuwa ni mganga kweli
kweli. Aliamua kumpeleka mke wake huyu Ukerewe ili apewe cheo kikuu cha
kufanya uganga. Mashekhe walimlazimisha mama huyu abadili dini lakini
akagoma. Baadaye walifanya dawa zao ambazo zilileta kizazaa kwa mtoto
mwingine wa mama huyu aliyemzaa na mume mwingine kabla ya kuanza
mahusiano na bwana huyu mganga. Hata hivyo bwana huyu alimpa
dawa/mitishamba mtoto huyu wa kambo na akapona.
Baadaye bwana
huyu alihamia Kiteto, kijiji cha Dosidosi ambako alimuita mke wake wakae
pamoja ili amsaidie kwenye kazi ya kuvuta wateja. Huyu mama alimfuata,
na kisha akawa na kazi ya kuandika maneno yote ya kiaguzi / kiganga
pindi wateja wanapokuja kufanyiwa uganga. Miongoni mwa dawa za mganga
huyu ni unyayo wa bata na kiini cha yai la bata. Kwa hiyo maisha ya
kula kuku-nyama yakamfurahisha sana huyu mama, na kujiona yupo salama.
Baadae siku moja baada ya kufanyiwa uganga usiku, ndipo tatizo la
kutokwa damu mfululizo likamuanza huyu mama.
Alipoona hali yake
ya kutokwa na damu inaendelea kumsumbua, alienda Hospitalini ambapo
alipata vipimo vyote, na kukutwa na magonjwa mengi tu kama vile typhoid,
Ukimwi, malaria kali, ukosefu wa damu n.k. Siku ya 69 baada ya damu
mfululizo kuendelea kumtoka huyu mama, aliletwa hapa kanisani (UFUFUO
NA UZIMA – MOROGORO) kuombewa, baaada ya kupewa ushauri huu na baba
mdogo wake anayeitwa Amani. Baada ya Maombi, damu yake ilifunga papo
hapo. Bwana wake alipiga simu siku hiyo hiyo akilaumu kwa nini
amepelekwa kanisani badala ya kupelekwa kwa mashekhe wawili kufanyiwa
tiba mbadala. Usiku wake huyu mama aliota ndoto kuwa amekutanishwa na
babu yake ambaye ni marehemu. Bwana wake akawa anampigia simu mkewe huyu
kusema, amemvurugia mambo yake. Mongoni mwa shutuma nyingine ni kuwa,
balaa zilikuwa zinaikumba sana familia ya huyu bwana, ikiwemo ajali za
pikipiki na moto kwa ndugu zake. Nyakati nyingine alimpigia simu mkewe
kumwambia eti Maombi ya Wakristo ni sawa na uchawi.
==USHUHUDA HUU SEHEMU YA PILI UTAENDELEA WIKI IJAYO==
==Na Mwandishi Wetu==
== Information Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)==
PICHANI: Cesilia akielezeea ushuhuda wake (part one) katika Nyumba ya
Ufufuo na Uzima - Morogoro Jumapili 06 April 2014. Kushoto kwake ni AP
Steven Nampunju na Kulia ni SNP (Baba) Godson Issa Zacharia wa Ufufuo
na Uzima - Morogoro
No comments:
Post a Comment