Saturday, October 5, 2013

AFUNGULIWA BAADA MIAKA KUMI NA MBILI YA MATESO (Ufufuo na Uzima Mega Crusade Arusha)

Dada Alberta Naftaeli Kihwelu, amepokea uponyaji wake katika Mkutano wa Mchungaji Josephat Gwajima jijini Arusha baada ya kuishi miaka kumi na mbili ya mateso. Muujiza huo umetokea baada ya kufika viwanja vya Relini, mahali ambapo mkutano wa kanisa la Ufufuo na Uzima unafanyika kwa siku ya tisa sasa.

Dada Alberta ambaye anaishi alikuwa anasumbulliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kukosa mafanikio katika kila alilokuwa akifanya; hatua ambayo ilimpelekea kunywa pombe kupita kisasi ambapo kwa siku moja alikuwa na uwezo wa kunywa chupa hadi 18 za bia na mara nyingine, sado mbili za pombe ya kienyeji bila kuhisi kulewa.

Aliendelea kueleza kuwa, kila ikifika muda wa saa tisa usiku husikia mtu anamwita jina lake nje ya nyumba yake na hujikuta amekimbilia maporini au mahali asipopajua. Na mara nyingine wakati wa usiku hujisikia kutoka nyumbani na kukimbilia barabarani na mara nyingi hukukoswakoswa na ajali mbaya.
Alberta (kushoto mwenye kanga shingoni) pamoja mdogo wake Lydia (aliyejifunika kitambaa cha batiki) 

Dada Alberta ambaye anaishi Moshi, aliendelea kusimulia kuwa siku moja aliwahi kukimbilia milimani na kukaa huko kwa muda wa wiki mbili akiwa analishwa nyama za ajabu asizozielewa na mtu ambaye alikuwa anamletea nyama hizo alikuwa hamtambui. Mateso hayo ameishi nayo kwa muda wa miaka kumi na miwili.

Dada Alberta ambaye alialikwa kwenye mkutano kwa kupigiwa simu na mdogo wake anayeishi Arusha aitwaye, Lydia Kihwelu. Akielezea hali ya dada yake; Lydia alisema kuwa kufika hapo uwanjani ulikuwa muujiza wa kwanza kwasababu alikuwa anakimbia ikabidi kumlazimisha kuja.

Pamoja na mateso hayo ya kutoroka usiku; dada Alberta pia alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya tumbo yasiyoisha kwa muda wa miaka kumi na miwili kila siku bila kupumzika. Alipofika mkutanoni akaombewa na kufunguliwa macho ya rohoni akajiona kuwa miaka yote hiyo alikuwa amechukuliwa kwa namna ya rohoni na jirani yake aitwaye Mr Kimambo; na kumweka katika banda lake la ng'ombe ili awalishe.

Baada ya maombezi makali kutoka kwa Mchungaji Gwajima pamoja na watendakazi wa Ufufuo na Uzima waliopo uwanjani, Arusha aliwekwa huru kabisa kutoka katika mateso hayo na maumivu ya tumbo yalimwacha saa ileile.

No comments:

Post a Comment